Sayansi ya Homoni na chakula: Ugumba,Nguvu za Kiume,Tezi dume,Fibroids na kansa

Sayansi ya homoni za kike na kiume na uhusiano wake na chakula

 Homoni ni kichocheo ambacho hutengenezwa na tezi mbalimbali mwilini. Na homoni husafirishwa na damu kwenda sehemu inapohitajika mwilini. Kumbuka kwamba kila homoni huwa ina kazi yake maalumu, huwezi kukuta homoni ya uzazi inaenda kuchochea umeng’enyaji wa chakula cha protini. Kila homoni na kazi yake maalumu.

Homoni kwa tafsiri nyingine tunaita ni “Kichocheo” kwa sababu madhumuni ya kutengenezwa kwa homoni ni kwenda kuchochea tendo flani la kibaolojia litokee mwilini.

Mfano: Homoni ya kike estrogen hutengenezwa na tezi iitwayo ovari na huenda kuchochea mambo mbalimbali kwa mwanamke kama kubarehe kwa mwanamke (Kuota matiti,Ngozi laini,nyoga kuongezeka,sauti nyororo), pia huchochea kujengeka kwa ukuta wa kizazi ili mimba ije ishike kwenye ukuta imara. Kwa maana hio homoni ni “Kichocheo cha mwili”.

Homoni zipo aina nyingi, kuna homoni za uzazi,usagaji chakula,zinazo ratibu matumizi ya wanga,mafuta na protein nk ila somo hili utajifunza homoni za uzazi kwa mwanaume na mwanamke.

Homoni ambazo zinachochea matukio mbalimbali ya uzazi kwa mwanamke ni Estogen,Progesterone,Prolactin, Follicle stimulating hormone(FSH),Luteinizing hormone(LH),na Testosterone.

Homoni hizi huwa zinatengenezwa na ovari kwa mwanamke lakini tezi inayo ratibu kiwango cha usawa wa homoni hizi ili isije ikatokea moja ikapanda sana na nyingine ikashuka sana. Kazi hio hufanywa na tezi iliyopo kwenye ubongo iitwayo Anterior Pituitary Gland. Kwa hio tezi hii inahakikisha kwamba hakuna homoni inayozidi wala inayopungua.

 

Kazi za homoni hizi:

 1. Estrogen
 • Huchochea matendo yote wakati ya kubalehe. Kuota matiti,Ngozi kuwa laini,sauti,nyoga kuongezeka nk
 • Hujenga ukuta wa kizazi ili mimba ije ijishike kwenye ukuta mnene.
 • Huchochea ukuaji wa matiti wakati una mimba.

 

 1. Progesterone
 • Hutengenezwa na tezi ya dharura (corpus luteum) pale ambapo yai limetoka
 • Kazi yake kubwa ni kulea mimba inaongezeka sana baada ya siku ya kupevuka kwa yai na baada ya mimba kutungwa.
 • Endapo mimba isipotungwa homoni hii inayoshikilia ukuta usibomoke hushuka kiwango chake na ndipo inawezesha ukuta kuporomoka kwa kutoa uchafu (damu) ili kwamba ukuta mwingine ujengwe kwa mzunguko ujao
 • Pia hukuza matiti wakati una mimba na kuendelea kufanya ukuta wa kizazi uwe imara sana

 

 1. Prolactin
 • Hii ni homoni ambayo hupanda sana wakati una mimba na unakaribia kujifungua
 • Hutengeneza maziwa yakutosha ili uweze kunyonyesha
 • Huwa ina mkinga mama asipate mimba mapema akiwa ananyonyesha. Ukiwa unanyonyesha homoni hii huwa nyingi na huzuia upevushaji wa mayai. Ila unashauriwa baada ya wiki sita tangu umejifungua kuwa makini maana kwa unyenyeshaji wa nadra kwa wanawake wengi unasababsha prolactin kutokuwa katika kiwango toshelevu kuzuia upevushaji wa mayai.

 

 1. Testosterone
 • Tunaita hii ni “homoni ya kiume” kwa sababu huwa ndio imetawala (inajionesha kuwa juu) kwa mwanaume kuliko homoni zingine. Lakini wanawake pia huwa wana hii homoni katika kiwango kidogo sana. Wao homoni inayo tawala ni estrogen.
 • Homoni hii inasaidia sana uhifadhi wa mafuta mwilini, pia inasaidia katika utumiaji wa vyakula vya mafuta,protini na wanga, pia inasaidia sana kutengeneza misuli ya mwili wako. Hivyo ni ya muhimu sana kwa mwanamke.

 

 1. Follicle Stimulating Hormone (FSH)

Hii ni homoni ambayo inakomaza mayai, na huanza kupanda kwenye damu siku ya kwanza tu umeanza kuingia hedhi. Yenyewe inaanza kuandaa yai ambalo litapevuka siku ya 14 katika mzunguko wako.

 

 1. Luteinizing hormone (LH)

Ni homoni ambayo husaidia yai liweze kutoka kwenye kiwanda yaani ovari na ndipo lije kwenye mirija ya uzazi kwa ajili ya urutubishaji.

 

 

Mambo ya Kuzingatia juu ya umuhimu wa homoni hizi

 

 1. Homoni hizo zote kwa mwanamke hutengenezwa na ovari na malighafi ya utengenezaji ni kiini lishe kiitwacho cholesterol au lehemu.
 2. Homoni zote hizo kiwango chake huratibiwa na tezi iitwayo Pituitary gland, na njia nyingine za kudhibiti homoni moja isipande sana huwa tunaita “Negative feedback inhibition” yaani pale ambapo homoni moja imeongezeka au inajitosheleza taarifa inapelekwa kwenye ubongo (pituitary) ili isitengeneze au itengeneze kidogo. Njia hii ndio wanasayansi walitumia kuweza kutengeneza vidonge,sindano na pandikizi za uzazi wa mpango. Hizo ni homoni ambazo zinaenda kuzuia tezi ya pituitary isitengeneza homoni zinazo komaza mayai na kupevusha mayai yaani FSH na LH hazitatengenezwa.

 

Je nitajuaje homoni zangu zipo vizuri?

 

Kuna kipimo cha maabara unachokuliwa sampuli ya damu na mtalamu wa maabara ataenda kufanyia kazi damu yako na kukuletea majibu baada ya siku moja mpaka mbili unaweza pata majibu.

Homoni za mwanamke huwa zinapanda sana kuanzia muda wa kubalehe na zinaanza kushuka pale unapo elekea kwenye kikomo cha hedhi miaka 50.

 

 

Kuvurugika kwa homoni maana yake ni nini?

 

Maana yake ni kwamba homoni zako haziko katika mhimili unaotakiwa na zinasababisha kwa namna moja au shinyine mzunguko wako wa hedhi unakuwa sio salama na linaweza kusababisha kutobeba hata mimba, inategemea na ukubwa wa tatizo lako.

 

Tizama mifano hii hapa chini

 1. Endapo homoni ya estrogen ikiwa juu sana inaweza kukuhatarisha pata magonjwa yafuayo;
 • Shinikizo la damu

Hii ni kwa sababu homoni ya estrogen huenda kuishinikiza figo kuzuia madini ya chumvi (sodium) yasitoke nje. Na kadri unavyozuia madini haya ya chumvi yasitoke huenda sambamba na kuzuia maji. Hivyo hii inaweza kupandisha kiwango cha damu (plasma) na kusababisha Shinikizo la damu,moyo kupanuka, kuvimba miguu nk

 

 • Kansa na uvimbe kwenye kizazi(fibroids)

Homoni hii huenda kuchochea seli za titi, ukuta wa kizazi kukua kwa kasi sana na zinaweza kuchochewa na kubadilika kuwa kansa. Hivyo homoni nyingi ya estrogen inakuweka hatarini kupata kansa ya titi (breast cancer), kansa ya kizazi (Endometrial cancer) na baadhi ya kansa za Ubongo.

 1. Homoni ya progesterone inapokuwa chini sana inaweza kusababisha yafuatayo
 • Kuwa na maumivu makali sana ya hedhi
 • Kuingia hedhi yenye kuambatana na kutokwa na damu nyingi sana na kwa muda mrefu
 • Mimba kuwa zinatoka, kila unapobeba mimba inatoka hata kabla haijamaliza miezi 3.
 1. Homoni ya Prolactin ikiwa juu sana kwenye damu unaweza kupata matatizo yafuatayo kiafya
 • Kumbuka homoni hii inapanda unapokuwa una mimba na unanyonyesha tu. Lakini ukikuta ipo juu sana kwenye damu wakati hunyonyeshi na huna mimba kiafya inakuwa sio salama.
 • Inaweza kusababisha kutokwa na maziwa wakati huna mimba na hunyonyeshi. Chuchu zikawa zinatoa maziwa.
 • Huwezi kubeba mimba kabisa kwa sababu prolactin ikiwa juu wakati huna mimba huenda kuzuia ovari zisikomaze na zisipevushe mayai kabisa. Unakuwa unaingia hedhi ambayo hairutubiki.
 • Matiti kuwa yanajaa na kuuma sana hasa unapokaribia hedhi
 1. Homoni ya testosterone ikiwa juu kwa mwanamke unaweza kupata madhara yafuatayo kiafya;
 • Kutokuwa unapevusha mayai hata kidogo hii inaweza kusababisha ukawa mgumba.
 • Mayai yanakuwa hayapevuki na matokeo yake unapata aina ya uvimbe kwenye ovari tunaita “Cysts”. Ambapo cyst inaweza kuwa moja na kubwa au zinaweza kuwa nyingi “Polycysts”. Kwa hio unakuwa hatarini kupata uvimbe kwenye ovari.
 • Kuota nywele sehemu ambazo mwanamke hutakiwi kuwa na nywele.Mfano ndevu kwa mwanamke, nywele kifuani nk
 • Hamu ya tendo la ndoa hupotea kwako inakuwa ni maumivu tu wakati wa tendo la ndoa.

 

Je kwa wanaume inakuwaje hili tatizo la mvurugiko wa homoni?

Wanaume pia huwa wanakabiliwa sana na matatizo haya ya mvurugiko wa homoni na huenda kuathiri sana uzazi kwa mwanaume.

 

Mfano

 1. Homoni ya Testosterone ikishuka kwa mwanaume unapata matatizo haya
 • Unaongezeka uzito kwa kasi hasa kitambi cha tumbo la chini,nyonga na mapaja na kupungua inakuwa kazi sana
 • Hamu ya kushiriki tendo la ndoa na matamanio kwa jinsia tofauti inapungua sana au kuisha kabisa inategemea na kiwango cha ukubwa wa tatizo.
 • Kiwango cha mbegu na ubora wa mbegu za kiume kushuka sana.
 • Unaanza kupoteza nywele, unaanza kukonda sehemu zingine isipokuwa tumbo la chini linaongezeka. Testostrone kujenga misuli ikiwa chini unaanza kupoteza misuli.
 1. Homoni ya estrogen ikizidi kwa mwanaume matatizo haya unapata
 • Homoni ya estrogen huwa ipo chini sana kwa mwanaume. Inapozidi kiwango yaani ikatawala inakufanya mwanaume matiti yakue,kitambi, unatengeneza hipsi kama mwanamke, na maumbile sehemu za siri yanaanza kupungua kwa kasi sana.
 • Inamhatarisha mwanaume tezi ya kiume kukua kwa kasi sana na kuanza kusababisha mkojo kutokutoka katika umri mdogo sana. Kitalamu Bladder outlet obstruction huwa tunatarajia uanze kupata ukiwa na miaka Zaidi ya 80 lakini kwa sababu ya homoni hii imetawala baadhi yetu tezi inakuwa kwa kasi sana. Hivyo tezi dume ukuaji wake hutegemea sana homoni hasa homoni ya estrogen. Hivyo unakuwa hatarini kupata BPH (Tezi inakua sana na kuzuia mkojo katika umri mdogo), na Unaweza kuwa hatarini kupata kansa ya tezi dume.

 

 Je kuna uhusiano gani kati ya chakula unachokula na kuvurugika kwa homoni za kike na kiume?

 Ushawahi kwenda hospitali una mvurugiko wa homoni ukaambiwa unywe juisi za matunda asili eti utapata vitamin ambazo zitaweka homoni zako katika usawa? Ushawahi kuambiwa ujichue kwenye uume wako wewe mwanaume eti kwamba utarudisha nguvu za kiume milele? Ushawahi kuambiwa nyama inachangia kuvuruga homoni na hukuza tezi ya kiume kwa kasi sana? Na ushawahi kuambiwa uache kula nyama mayai kwa sababu vina mafuta kula dona,wali,mikate ya ndano kwamba havina sukari utapungua na utaweka homoni katika usawa? Sintofahamu hii ndio imenifanya niandike Makala hii.

 

Asilimia kubwa ya homoni hizi kutoka kwenye mhimili wake kutokana na uzoefu wangu kwa miaka Zaidi ya 4 sasa nikiwasaidia maelfu ya watu kula kiafya na nikitafiti kwa kina kuhusu mpangilio sahihi wa chakula kwa binadamu ni upi, Asilimia kubwa ya watu wanateswa na Lishe mbovu.

 

Sasa wengi hawaelewi na hawajawahi kutaka kutengua kitendawili hiki “Lishe bora maana yake ni mpangilio upi? Maana kuna wengine wanaamini wanakula lishe bora angali wanaumwa maradhi karibia yote ya lishe na hawastuki yawezakuwa wanapotea njia wako kwenye lishe mbovu”

 

Nimejaribu kuchunguza kwa kina uhusiano wa sukari, wanga na idadi mingi ya milo pamoja na mafuta mabaya ya mbegu za mimea hasa ya mgando nimegundua kwamba kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mvurugiko wa homoni na vyakula hivi.

 

Mfano hebu tuangazie uhusiano kati ya homoni na vyakula vya wanga na sukari.

 

Mwili wa binadamu umetengenezwa kujiendesha katika mazingira ya kiwango kidogo sana cha sukari. Kiwango salama cha sukari kinachotakiwa kuendesha mwili muda wote ili isitokee shida yoyote kiafya ni 5.6mmol/l au 100mg/dl.

Kwa sababu damu ya binadamu inakadiliwa kuwa ni lita 5 mpaka 7 hivyo ukifanya mahesabu hapo ina maana kiwango cha sukari kwenye damu kinatakiwa kiwe gram 5 kwenye lita 5 za damu. Ukienda kiuhalisia Zaidi gram 5 ya sukari ni sawa na kijiko kimoja kidogo cha sukari.

 

Tafsiri yake ni kwamba sukari inayo endesha mwili wako usianguke kitalamu inatakiwa icheze gram 5 mpaka 10 ambapo ni sawa na kijiko 1 mpaka 2 basi. Soda moja inakadiliwa kuwa na gram 37 sasa gawanya kwa 5 upate idadi ya vijiko ulivyo mimina mwilini utapata vijiko 7. Haya wewe umekula ubwabwa wa jana,chapati mbili na juisi nachuro ya embe au tikiti grasi moja au mbili. Mwili wako utashukuru kwa upendo na huruma ila utabadilisha sukari yote iliyozidi kuwa mafuta. Na mwili utapigana kuhakikisha kwamba hata kama sukari ilikuwa imepanda kwa kiwango gani ndani ya masaa 2 sukari lazima iwe inasoma kijiko 1 mpaka 2 kwenye mwili wako wote.

Je unafahamu madhara ya kuupendelea mwili wako na sukari na uhusiano wake na homoni za kiume na kike?

 Pale tu unapomimina sukari nyingi mwilini, pale tu unapomimina wanga kwa wingi mwilini. Kongosho lako huwa linaamka kwa kumimina insulin nyingi kwenda kuratibu matumizi ya hio sukari na yote ambayo haina matumizi husukumwa kuwa hifadhi mwilini yaani Glycogen na mafuta kwa asilimia kubwa. Mafuta ni tenki la kuhifadhi sukari ya ziada ambalo huwa halina ukomo, yaani kadri unavyoweka sukari ndivyo mafuta yanavyozidi kukufinyanga katika umbo la aina yake. Haipo siku tenki la mafuta huwa linajaa, wewe weka sukari kwa uwezo wako itabadilishwa na kuwa mafuta na kukufinyanga umbo utakalo.

Kadri unavyozidi kuhiafadhi mafuta mabaya mwilini, huwa yanaanza kuleta mashambulizi mwilini na kudumaza mwili wako. Kadri mwili wako unavyodumazwa na mafuta hayo ya ziada mwili wako unapoteza uwezo wa kutumia sukari kama kawaida. Kupungua kwa ufanisi wa seli za mwili wako kutumia sukari hio hali tunaita Insulin resistance.

 

Ooooo! Hebu tulia kwanza nimekupa msamiati mpya ee! Nakufafanulia Rafiki yangu sitaki ukose mwafaka leo wa tatizo lako. Insulin resistance ni ile hali seli za mwili wako zinapoteza uwezo wa kutumia sukari vizuri. Ili sukari iweze kutumiwa na seli ya mwili wako,insulin huwa inafanya kazi ya kuishinikiza seli itumie sukari, na insulin hufanya kazi hio kwa kugusa ukuta wa seli kisha seli inaitikia kwa kuruhusu sukari iingie ndani na itumike. Sasa unapokuwa na insulin resistance hata kama insulin ipo nje imegusa ukuta wa seli, basi hio seli inagomea wito (signal) ya kuruhusu sukari iingie kwenye seli. Matokeo yake hali hii inaendelea kujengeka siku na siku mpaka inafikia hatua mbaya Zaidi na kuitwa mgonjwa mwenye kisukari rasmi.

 

Ukiwa katika hali hio mwili ukisha hifadhi mafuta mengi,umedumaa,umechakaa seli zimetengeneza insulin resistance katika kiwango kikubwa. Kongosho lako linakuwa halikubali kushindwa kushusha sukari. Linakuwa linamwaga insulin nyinyi nyingi nyingi ili insulin hio ikaondoe kizuizi katika seli na sukari iweze kushuka. Hatua hio ya kongosho linapokuwa linatema insulin nyingi kukunusuru wewe usiugue kisukari huwa ni hatua ya utahiniwa wa kisukari kitalamu tunaita prediabetes.

 

Sasa basi hali hio ya mwili wako kuhatarishwa kuwa katika kiwango kikubwa cha insulin muda wote kitalamu tunaita “Chronic hyperinsulinaemia” husababisha sukari kuwa inashuka mara kwa mara, ndio maana watu wanene huwa wana njaa kali sana kwa sababu pale tu wanapokula chakula,mwitikio wa kongosho huwa ni wakishindo na hio huenda kushusha sukari haraka sana. Njaa za mtu mnene ni kali na muda wote ana njaa.Pia hali hii inamsababishia asipungue kabisa kwa sababu homoni ya insulin ikiwa juu huwa inashikilia mafuta. Kwa maana hio unapopata Insulin resistance ni kama tiketi ya maradhi makubwa Zaidi, njaa zinakuwa kali, na unanenepa kwa kasi na kupungua inakuwa ngumu maana mafuta yameshikiliwa.

Sasa tuone athari za mwili wako kuwa katika hali hii ya Insulin resistance katika homoni.

Insulin rsistance kwa lugha nyingine huwa tunasema ni mzizi wa maradhi karibia yote ya lishe. Na moja ya dalili kubwa kwenye damu ni “Chronic hyperinsulinaemia” yaani nikikupima homoni ya insulin kwenye sampuli ya damu ukiwa haujala (Fasting insulin assay) lazima itakuwa iko juu kuliko kawaida inavyotakiwa kiafya. Mtu yeyote aliyepo kwenye hali hii huwa yupo kwenye utahiniwa wa maradhi yote ya lishe. Asilimia kubwa wanaohangaika na matatizo ya homoni, nguvu za kiume,uvimbe kwenye ovari na kizazi huwa wapo hapa.

 

Mwili wako unapo uhatarisha katika kiwango kikubwa cha insulin kwa sababu ya huruma yako ya ajabu,kumimina sukari nyingi kuliko mahitaji ya mwili. Matumizi mabaya ya vyakula vya wanga na sukari husababisha yafuayo katika homoni za mwanamke na mwanaume.

 

Kwa mwanamke:

 1. Homoni ya insulin huchochea utengenezaji wa homoni ya testosterone ambayo kwa mwanamke inatakiwa iwe chini. Sasa ulaji wa vyakula vya wanga na sukari unachochea hali hii. Na homoni hii huchochea kutokea kwa uvimbe kwenye ovary (cysts) n ahata kuzuia kukomaza na kupevusha mayai. Hivyo huwezi kubeba mimba.
 2. Homoni ya kiume inapokuwa juu kwa mwanamke wakati haitakiwi iwe hivyo. Mfumo wa kudhibiti kiwango cha homoni mwili huanza kazi ya kuirudisha katika usawa. Njia pekee ni kuichukua hio testosterone na kuibadilisha kuwa estrogen haraka sana kazi hio hufanywa na aromatase. Na kitendo cha kubadilisha testosterone kuwa estrogen tunaita kitalamu Aromatization. Chakula cha wanga na sukari huchochea sana aromatase enzyme ifanye kazi kwa kasi sana nah ii husababisha Estrogen kupanda kwenye damu.
 3. Ni kawaida unapochukuliwa sampuli ya damu kwa mama mwenye Polycystic ovarian syndrome kukuta homoni ya progesterone iko chin sana, homoni ya testosterone iko kawaida kwa sababu yote inabadilishwa haraka sana kuwa estrogen kupitia kitendo cha aromatization. Kwa hio majibu ya kipimo cha homoni yataonesha homoni ya estrogen ndio iko juu. Nishawahi kuwa na mgonjwa wa namna hii, testosterone ilikuwa kawaida, estrogen iko juu na progesterone iko chini na alikuwa hashiki mimba. Ila baada ya kushughulikia testosterone kwa lishe ikashuka, estrogen ikarudi kawaida na akabeba mimba.
 4. Ndio maana kumtibu mama tatizo la homoni kwa kumchoma sindano za homoni au kumnywesha vidonge vya uzazi wa mpango (homoni) hakuwezi kutoa suluhu. Kwa sababu unapo upatia mwili homoni za nje ubongo wako katika pituitay unabaini uwepo wa homoni hzio kwenye damu hivyo unazuia kutengeneza homoni ya kukomaza na kupevusha mayai. Kadri unavyozidi kunywa au kuchoma itafikia hatua haziwezi kuchochea kazi yake kama ilivyokuwa awali “Hormonal resitance” hii inaweza kumsababishia daktarin akawa anakuongezea dozi ya homoni kila siku na tatizo linakomaa kila siku.
 5. Homoni ya estrogen inapokuwa nyingi sana kwa mwanamke hali hio inakuhatarisha kupata kansa ya titi, uvimbe kwenye kizazi yaani fibroids na pia kansa ya kizazi. Ndio maana wakina mama wengi baada ya upasuaji wa fibroids huendelea kula vibaya akijua shida ameshaondoa maana ameondoa labda kizazi. Kumbuka aina hizi za uvimbe na kansa zinamea kwa kasi kwa kutegemea homoni, umeondoa uvimbe kwenye kizazi, umeondoa kizazi umeondoa titi ila hujarudisha homoni zako katika kiwango (balance) inayo takiwa. Hivyo lazima lishe uzingatie na utafiti uone kuna uhusiano gani kati ya mfumo wako wa kulan a hayo maradhi ili usije tena ukajihatarisha na magonjwa mengine yenye kisababishi kimoja.

 

Kwa mwanaume:

 

Kwa mwanaume kiwango kingi cha homoni ya insulin kwenye mwili wa mwanaume kwa sababu ya matumizi mabaya ya wanga na sukari na katika idadi ya milo mingi. Huchochea sana kitendo nilicho zungumzia hapo juu cha utenegenezaji wa homoni za kike kwa wingi yaani Estrogen. Kwa mwanaume homoni hii inaanza kutawala kwenye damu.

Haya ndio madhara yake kwa afya ya mwanaume

 1. Homoni ya estrogen inapokuwa juu sana inashusha hamu ya tendo la ndoa kwa mwanaume kabisa, maumbile yanakuwa yanapungua kila siku. Ndio maana huwa nawapa somo unapopungukiwa nguvu za kiume na maumbile yanapopungua shida huwa ipo kwenye homoni. Lakini dawa nyingi ni za kusisimua misuli ya uume badala ya kushughulikia homoni.
 2. Homoni ya estrogen huenda kushinikiza figo kuzuia madini ya chumvi na maji. Na hii inaweza kusababisha presha ya kupanda, moyo kupanuka nk
 3. Uwezo wa kutungisha mimba wewe mwanaume unashuka sana kwa sababu idadi ya mbegu inashuka na ubora au afya ya mbegu inakuwa chini sana
 4. Tezi ya kiume huwa inakuwa kwa kasi sana kwa kutegemea homoni hii, ndio maana hata dawa za tezi dume huenda kushusha kiwango cha estrogen kwa kuzuia aromatase isifanye kazi yake ya kubadilisha testosterone kuwa estrogen. Hivyo kiwango kingi cha homoni hii kwa mwanaume inakuhatarisha tezi dume kukua kwa kasi sana na kuanza kuzuia mkojo usitoke katika umri mdogo. Pia hata kansa ya tezi dume unakuwa hatarini kuapata.

 

Mambo ni mengi sana kwa nini homoni zinavurugika ila kwa asilimia kubwa ni lishe na mvurugaji mkubwa sana anayetesa ndoa nyingi ni vyakula vya wanga na sukari. Asilimia kubwa sana ya wanawake wagumba ni kwa sababu hawataka kubadilisha mfumo wao wa kula, na hii ndio sababu inayowafanya waanze kutumia njia za mabavu kusawazisha homoni kama kutumia sindano za homoni za kike na sindano za kiume.

Mfano wanaume wengine huamua kuchukua hatua ya kuchoma sindano za testosterone, lakini sayansi inatuonesha kwamba hautakuwa umepata suluhisho. Kwa sababu kadri unavyozidi kuchoma mwili hutafuta mbinu ya kuipunguza kwenye damu na njia moja wapo ni kuichukua hio testosterone na kuibadilisha kuwa estrogen kitendo hicho huitwa aromatization. Ina maana wewe unakuwa unajipumbaza unaongeza homoni za kiume kumbe hapo hapo mwili unapambana kui-balance na kufanya hivyo kunakupandishia homoni ya kike wewe mwanaume.

Njia nzuri na imara kuiboresha ndoa yenu ni kubadilisha mfumo wa kula, familia nyingi tunakula hovyo sana, na wengi tunapuuza kwamba yawezakuwa chakula ndio kinaleta migogoro ya kifamilia. Mfano tafiti zinaonesha kwamba homoni zinapovurugika kwa mwanamke na kusababisha estrogen ikawa juu na testosterone ikashuka, huwa inamhatarisha mwanamke kupata maambukizi ya mara kwa mara na sugu yenye kumsababishia kupata uchafu wa kudumu usiokoma unaotoka muda wowote katika uke. Hivyo hii inaweza kupoteza kujiamini kwa mwanamke kwenye tendo la ndoa,msongo wa kudumu,kujikatia tamaa na kama ni wana ndoa basi mifarakano katika ndoa.

Kwa sababu mama ndiye mpishi wa nyumbani, na mama ndiye huwa mtu wa kwanza kutafuta tiba hii kuliko wanaume, kwani wanaume wengi huwa hawataki kukiri wana shida katika uzazi wake hasa nguvu za kiume, na kama ni kwa mwanamke huwa hawataki kabisa kuonekana na mapungufu hayo. Sasa nitakuomba zoezi la kubadilisha familia lianzie kwako,kisha kwenye manunuzi ya vyakula,kwenye mapishi na jinsi unavyo pangilia chakula chako jikoni. Nina Imani wengi mnaoteseka na matatizo haya kama tatizo ni lishe basi sayansi ya mapishi itakusaidia. Ninapokea shuhuda nyingi sana juu ya uponyaji wa tatizo hili ndio maana nimeamua kuandika Makala hii kuelimisha jamii kwa undani kidogo juu ya mchango wa vyakula katika Kuvuruga ndoa yenu.

 

Soma Kitabu cha SAYANSI YA MAPISHI utajifunza namna ya kujikinga na maradhi na migogoro ya kindoa inayo sababishwa na lishe mbovu. Epuka tabia ya kula chochote kinachopita kwenye paji la uso wako,kinaenda kukugombanisha na mumeo na mke wako.

Tizama video zangu za Mafunzo haya;

SEHEMU YA PILI YA SOMO

 

SOMA SAYASI YA MAPISHI UANZE SAFARI YAKO

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*