Sayansi Ya Mafuta na Cholestrol: Matumizi ya mafuta,Cholestrol, Sifa ya Mafuta salama

 MCHANGANUO WA VYAKULA VYA MAFUTA

 Ushawahi kuambiwa mafuta hayahitajiki katika lishe yako? Na mafuta huleta magonjwa ya moyo kwa kuongeza cholesterol kwenye damu? Pia ukaamini kwamba vyakula vya wanga ni chanzo kikubwa chenye kukupatia nishati nyingi kuliko vyakula vya mafuta. Yote hayo yawezakuwa ni uongo na umeyapokea kwa kutojua misingi ya sayansi.

Sifa kubwa ya vyakula vya mafuta huwa ni “Kutochangamana na maji” kwa sababu mafuta huwa ni mepesi kuliko maji.

Mafuta yanapewa jina la pamoja katika lugha ya kisayansi maarufu kama “Lipids” hivyo unaposoma ukakutana na neno “Lipids” tambua kwamba mwandishi anazungumzia mafuta. Ambapo pia unaweza kulifafanua zaidi jina hili kwa kusema ndani ya jina Lipinds tuna aina kuu mbili ya mafuta ndani yake “Fat na Oil”.

Ambapo Fat humaanisha kwamba mafuta katika mfumo “Yabisi/Magumu” na Oil humaanisha mafuta ambayo yapo katika mfumo “Kimiminika” katika joto la mazingira ya kawaida.

Mfano wa mafuta ambayo huitwa fat ni kama samli,siagi nk na mafuta ambayo ni oil ni kama alizeti,pamba,mahindi,soya nk

Mafuta tunayopata kupitia chakula hujulikana kwa jina la “Triacylglycerol” hufupishwa kwa herufi tatu “TAG” au jina jingine “Triglycerides” hufupishwa kwa herufi tatu pia “TGA”.

Mafuta haya huwa yanapokuwa yamefungamana pamoja, yameundwa na viini vikuu viwili ambavyo ni Glycerol ambacho ni kiini kitengenezacho uti wa mgongo wa mafuta na kiini cha pili ni Fatty Acid.

Ingawaje katika kutengeneza umbo la mafuta (TAG) unatakiwa utambue kwamba kila Kiini kimoja cha Glycerol huwa kinaungana kwa kubeba viini vya Fatty acid vitatu na kutengeneza “Muungano/Bond” uitwao kitalamu “Ester bond” ndio maana mafuta haya hupewa jina la “Triacylgycerol” neno hili ni la kiratini likimaanisha viini vitatu vya Fatty acid vimeungana na glycerol kwa kutengeneza “Bond” kwa kitalamu tunaweza kufafanua zaidi ni “Triester of Glycerol and Fatty Acid”.

Lengo la kukueleza jinsi muungano huu unavyotokea hadi kutengeneza mafuta (TAG) ni kwamba pale unapokula vyakula vya mafuta kinapoanza kumeng’enywa katika mfumo wa chakula kinachofanyika ni vimeng’enya chakula (digestive enzymes) huvunja huo muungano (Bond) na tunapata zao la mwisho kwenye mfumo wa chakula huitwa FATTY ACIDS na GLYCEROL

 

MCHANGANUO WA MAFUTA

Mafuta unaweza kuyachanganua kwa kutumia njia nyingi sana,nitapenda ujifunze njia hizi ambazo zinatumika mara kwa mara katika kuchanganua mafuta

 1. Uwezo wa Kustahimili joto la mazingira husika na mfumo wake katika mazingira hayo

Hapa tunapata aina mbalimbali ya mafuta kwa kutumia sifa ya uwezo wa mafuta kustahimili au kutostahimili joto katika mazingira na sifa hio ndio inayo athiri hata mfumo wa mafuta hayo.

Mfano,Mafuta ya ng’ombe na mafuta ya alizeti. Mafuta ya ng’ombe yapo katika hali yabisi/ngumu ukilinganisha na mafuta ya alizeti ambayo ni kimiminika katika mazingira ya joto la kawaida.

Kutokana na sifa hio tunapata aina kuu mbili za mafuta kama zifuatazo;

 

 1. MAFUTA YENYE SIFA YA MGANDO (SATURATED FATS)

 

Sifa zake:

 1. Haya ni mafuta ambayo huwa ni mgando katika joto la kawaida katika mazingira yetu ya kila siku.
 2. Mafuta haya kwa sababu yanastahimili joto sana huwa hayawezi kuharibika ubora wake mapema. (Ubora wake unadumu kwa muda mrefu) na tunaposema mafuta kuharibika ni pale yanapoanza kutengeneza sumu ziitwazo peroxides na aldehydes na kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
 • Mafuta haya pia huwezi kuyabadilisha kwenda katika mifumo mingine ya mafuta kama vile unavyoweza kuyabadilisha mafuta yatokanayo na mbegu za mimea (Seed oils) kwa kuyapasha katika tanuru la moto mkali kutumia zoezi maarufu kama “Hydrogenation”. Kitendo hiki huhusisha kuongeza hydrogen atom kwenye mafuta husika. Lakini mafuta haya huwa yanajitosheleza na hydrogen atom kimuundo kwa hio huwezi kuongeza hata kama ukitumia joto la namna gani.
 1. Hakuna nafasi ya hizo hydrogen atom zitakapo enda kukaa katika umbo la mafuta yanayoganda.
 2. Kuganda kwa mafuta haya ni asili yake kimuundo. Haimaanishi kwamba binadamu ameyatengeneza yaakanza kuganda.
 3. Mfano wa mafuta ambayo huwa mgando asili ni samli,siagi,nazi na mfano wa mafuta ambayo sio salama kwa afya kwa sababu yametengenezwa na binadamu kuwa mgando ni bidhaa zote zilizotengenezwa kwa margarine.
 • Mfano wa mafuta haya ni Mafuta yatokanayo na Nyama,Maziwa,Nazi,Siagi,jibini kiujumla ni mafuta mengi yatokanayo na wanyama huwa yana sifa hii.

 

Utashangaa unashauriwa kuacha kutumia mafuta mgando asilia na unaambiwa kutumia mafuta mgando ya kutengenezwa kiwandani na binadamu kwa kutumia mafuta ambayo hayana tabia ya kuganda (vegetable oils). Ni hatari sana kiafya kama tulivyojifunza mwanzo.

 

 

 1. MAFUTA YENYE SIFA YA KIMIMINIKA (UNSATURATED FATS)

 

Haya ni mafuta ambayo yapo katika mfumo wa “Kimiminika katika mazingira ya joto la kawaida”

 

Sifa zake

 1. Huwa ni kimiminika katika joto la Kawaida unaweza kutumia neno “Oil”
 2. Chanzo chake kikuu ni Mbegu za mimea kama soya,mahindi,pamba,alizeti nk
 • Mafuta haya huwa yana upungufu wa “hydrogen atom” ndio maana yamepewa jina la “Unsaturated fats” kwa maana hio unaweza kutumia mbinu ya kubadilisha mafuta haya kuwa mgando, iitwayo kitalamu “Hydrogenation”
 1. Hydrogenation hufanyika kwa kuongeza atomu za hydrogen kwenye mafuta kwa kutumia joto kali sana huku ukisaidiwa na nickel, kemikali zinazotumika kurahisisha zoezi hilo zito na mwishoni tunapata mafuta yanayo ganda yatokanayo na mimea.
 2. Mafuta hayo hujulikana kama Transfats wengi hapa Tanzania huyapa jina la “Samuli itokanayo na Mafuta ya Mbegu za mimea” mimi huwa nayaita ‘Samuli chakubumba” maana sote tunajua mafuta ya samuli hutokana na maziwa ya ng’ombe iweje leo yatokane na chanzo kingine?
 3. Kwenye maduka utakutana na jina maarufu kama Margarine. Ingawaje zipo bidhaa za makampuni mbalimbali zinazotengeneza mafuta au chakula kwa kutumia margarine. Kuwa makini sana utaikuta kwenye keki,mikate, kupaka kwenye mikate ili kulainisha.
 • Mafuta ya margarine, yaliyopatikana kupitia kitendo cha kimaabara na kiwandani yaani hydrogenation “Mafuta yaliyochakatwa kiwandani kupindukia” kwa sababu ya kuhusisha mlolongo mrefu wa kubadilisha mafuta kutoka kwenye mfumo wa kimiminika na kuwa mafuta yabisi.
 • Hydrogenation huzalisha sumu nyingi ziitwazo “Free Radicals” ambapo ndio chanzo kikubwa cha magonjwa ya hivi karibuni Kitambi,kisukari,kansa,shinikizo la damu,moyo kupanuka na kuchakaa kwa mishipa ya damu,pumu,upungufu wa nguvu za kiume,Mzio (Allergy),kushambuliwa wa mifupa yako nk.
 1. Mafuta haya unaweza kuyakuta katika majina tofauti tofauti lakini majina maarufu ni “Margarine, Transfats, Partially hydrogenated fats” kwa sababu za kibiashara makampuni mengi yameacha kutumia neno Transfats na margarine maana wengi wamekuwa wakiziepuka bidhaa hizo na jina linalopatikana katika vyakula mbalimbali ni “Partially Hydrogenated fats”
 2. Mafuta haya kwa Tanzania unaweza kuyakuta katika vyakula mbalimbali mfano,Vitafunwa mbalimbali vinavyouzwa kwenye maduka ya vyakula mfano corn flakes,popcorn,biskuti,Frozen Pizza,Donut, mikate,keki pia katika mafuta ya kupikia na kupaka kwenye vyakula Blueband,Mafuta mengine ambayo sio salama ni Crisco oil.

 

Ulaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha free radicals, peroxides na aldehydes unauhatarisha mwili wako kuingia katika msongo wa sumu yaani oxidative stress na kuanza kushambuliwa na magonjwa ya mashambulizi ya kinga ya mwili ikiwemo kisukari, Magonjwa ya moyo,Pumu nk

 

Mafuta haya yaliyo katika mfumo wa kimiminika yanaweza kuchanganuliwa pia katika mifumo mingine kama hivi;

 

 1. Monounsaturated Fats

Haya ni mafuta ambayo yapo katika mfumo wa kimiminika na huwa yanaupungufu wa hydrogen atomu 2 tu (Pea moja ya hydrogen atomu).

 

Mafuta haya ni Olive oil, Karanga,Mawese, Mafuta ya Almonds, Mafuta ya Parachichi

 1. Mafuta haya yanafaa sana hata kutumia moja kwa moja kwenye chakula bila hata kupitisha kwenye moto ndio maana wengi hufanya mafuta haya kuwa ni sehemu ya vitu muhimu katika meza ya chakula kwa kunyunyuzia chakula chako mara tu baada ya kukamilika kabla ya kuanza kula.
 2. Mafuta haya huwa hayastahimili moto mkali ndio maana hatushauriwi kuyatumia kukaangia chakula kwenye mafuta mengi kwa muda mrefu. Utakuwa unatengeneza sumu nyingi sana.
 • Kumbuka mafuta yanasaidia sana umeng’enyaji wa chakula katika mfumo wa chakula. Usipoweka mafuta ya kutosha kwenye chakula chako sio tu mfumo wako wa chakula utakuwa sio wenye afya bali pia utapata matatizo kama choo kigumu, gesi au kutopata choo kabisa. Mafuta ni sehemu ya lishe bora tumia mafuta kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa katika kitabu hiki.

 

 1. Polyunsaturated Fats

Haya ni mafuta ambayo yapo katika mfumo wa kimiminika na huwa yana upungufu wa atomu za hydrogen zaidi ya pea moja.

Mafuta haya ni Alizeti, Soya, Pamba, Mahindi (Corn Oil),Canola oil.

 1. Mafuta haya kimuundo yana kiwango kingi cha uwiano wa omega 6 ukilinganisha na omega 3. Ndio maana wagonjwa wangu wote huwa siwashauri kutumia mafuta haya kwani moja ya sababu ya kumaa kwa mwili ni pale mwili unapoingia kwenye msongo wa sumu yaani Oxidative stress. Pia tumejifunza kwamba kiwango kingi cha omega 6 huleta majeraha katika mwili na kudumaza mwili haraka hatima yake ni ugonjwa wa kisukari.
 2. Mafuta haya huwa hayastahimili joto na mazingira ndio maana hata katika usindikaji huwezi kukuta mtu kasindika chakula mfano Piza base kwa kutumia mafuta haya. Lakini pia mafuta haya hayastahimili moto mkali na sio vizuri kiafya kuchoma chakula chako kwenye mafuta mengi kwa kutumia mafuta ya mbegu za mimea. Utakuwa unatengeneza sumu nyingi sana.
 • Moja ya tafiti iliyofanyika kwa kukusanya mafuta kutoka nyumbani, kwenye migahawa na kwenye hotel kubwa na viwandani. Mafuta yalitoka nyumbani yalijikuta yana sumu ziitwazo peroxides na aldehydes kwa sababu ya kuyaunguza mafuta kwenye moto mkali. Lakini mafuta yaliyokusanywa kutoka hotelini na kiwandani yalikuwa na sumu nyingi Zaidi kwa sababu kwenye migahawa mikubwa na kiwandani mfano wanakaanga samaki,chips, kuku nk unakuta anatumia mafuta yale yale mpaka yaje yakauke yatakuwa yameungua kwa muda mrefu na kutengeneza sumu nyingi sana. (1)
 1. Mafuta haya huwa yanaanza kutengeneza sumu mapema sana kuanzia nusu saa baada ya kuwa kwenye moto mkali kuanzia nyuzi joto 180 na kuendelea. Hivyo chukua mfano mtu mwenye kibanda cha kuchoma chips,kuku,samaki anaweza lita 10 kwenye deep fryer (kikaango) anakaanga chakula chake akirudia mafuta haya mara kadhaa ili asiweze kupata hasara mpaka yananyauka. Kitendo hicho hutengeneza sumu nyingi sana na unahatarisha mwili wako kuingia kwenye msongo wa sumu.
 2. Mbali na jamii kufundishwa kwamba mafuta yanayo ganda huleta magonjwa ya moyo, na mbadala wake ni mafuta yasiyo ganda yaani kama alizeti,pamba, soya,mahindi nk. Ila sasa elimu hio imekuwa na mapungufu makubwa sana katika jamii yetu maana hatujaifundisha jamii namna ya kutumia mafuta haya yasiyostahimili moto na mazingira.
 3. Ingependeza sana jamii ikapewa onyo na maelekezo yakutosha kuhusu matumizi sahihi ya mafuta haya ya mbegu za mimea. Maana tafiti zinazidi kuongezeka zikihusisha magonjwa ya moyo na kiwango kingi cha sumu hizi zitokanazo na mafuta haya yasiyostahimili moto. Kuendelea kukaa kimya huku rundo la tafiti likionesha kwamba unapokuwa kwenye msongo wa sumu hizi mwili wako unakuwa hatarini kupata mashambulizi ya moyo muda wowote.(2) (3) (4) (5)
 • Mafuta ya mgando asilia kama Samli, siagi nazi nk hustahimili moto na yanaweza kufaa kwa matumizi ya nyumbani hata kwa kuchomea chakula katika moto mkali. Ina maana mafuta haya yanaweza kukinga na magonjwa ya moyo kinyume kabisa na ambavyo umekuwa ukiambiwa na wengi kwamba mafuta yanayo ganda huziba mishipa ya damu. Sayansi sio rahisi kiasi hicho!
 • Tafiti nyingi sana zinakanusha kisayansi kula mafuta yanayo ganda kunaweza kusababisha mishipa ya damu kuziba na ukapata shambulio la moyo. Nimejaribu kufuatilia tafiti na vitabu mbalimbali vya misingi ya sayansi hakuna ushahidi wa kutosha kutuaminisha kuna ukweli kisayansi mafuta huenda kurundikwa kama mafuta ndani ya mishipa ya damu na kutuletea magonjwa ya moyo. (6) (7) (8) (9)

 

Mchanganuo wa pili wa mafuta ni Kutokana na Umuhimu wake katika mwili wa binadamu

 

Katika aina hii ya mchanganuo tunatenga mafuta kutokana na umuhimu wake mwilini kwa sababu mwili hauwezi kuyatengeneza au unaweza kutengeneza mafuta hayo.

 

Mfano: Vyakula mahususi na Vyakula visivyo mahususi katika kitabu changu cha sayansi ya mapishi nimeeleza kwa kina kwa nini vyakula vya wanga na sukari sio mahususi na ndivyo tunavyokula kwa kiwango kikubwa.

 

Neno essential hapa linasimama kama ni lazima ule maana mwili hauwezi kutengeneza hicho na hakuna namna ya mwili kujipatia hicho kiini lishe isipokula katika lishe.

 

Neno non essential maana yake hapa ni mwili unaweza kutengeneza hakuna ulazima kwamba lazima ule ndipo uwezo kupata aina hio ya kiini lishe

 

Vyakula vya protini na Mafuta hujulikana kama ‘Essential Nutrients” yaani Vyakula ambavyo mahususi mwili ukiunyima hautakuwa salama maana kuna baadhi ya mafuta lazima mwili upate.

 

Tunapata makundi makuu mawili ya vyakula vya mafuta endapo tukichanganua kulingana na uhitaji wake katika mwili wa binadamu.

 

 1. Mafuta mahususi mwilini

Haya ni aina ya mafuta ambayo mwili wa binadamu hauwezi kutengeneza kitalamu hujulikana kama “Essential Fats” kwa mfano Linoleic, Linoleinic na Arachidonic asidi.

 • Linoleic hupatikana kwenye vyanzo kama Flaxseed, Walnut, Mbegu za maboga, nk
 • Arachidonic acid hupatikana katika vyanzo kama kama Mayai, nyama,kuku, samaki na kumbuka kwamba ingawaje Ini la binadamu linaweza kutengeneza ila huwezi kupata kiwango toshelevu.

 

Note:

Mafuta mahususi pia unaweza kuyatenga katika makundi mengine zaidi kama Omega 3, Omega 6 na Omega 9.

 

Mafuta haya yote lazima mwili upatie katika kiwango sawia cha uwiano wa 1:1 lakini tafiti zinaonesha kwamba tumekula kupindukia mafuta ya omega 6 kuliko omega 3 hadi zaidi ya uwiano wa 1:30.

 

Je tumezidishaje kiwango cha Omega 6?

 

Kwa sababu tunakula sana kiwango kingi cha vyanzo vikuu vya omega 6 ambavyo ni Alizeti, pamba, mahindi (Corn oil), canola oil nk. Pia tumesahau vyanzo vya omega 3 ambavyo ni samaki, mayai, nyama, karanga nk

 

Kutowiana huko kunasababisha miili yetu kutengeneza mzio ndani ya mwili “Low grade chronic inflammation” ambao tunaweza kuzima moto huu ndani ya mwili wako kwa kupunguza matumizi ya Omega 6 na Kuongeza omega 3. Na mcharuko huu wa mwili nimekuwa nikiona wateja wangu wengi wakisumbuka na shinikizo la damu, pumu, kitambi kisukari kwa sababu ya chanzi hiki.

 

 1. Mafuta yasiyo mahususi mwilini

Haya ni mafuta mabayo sio lazima upate ili uweze kuishi bila shida yoyote kiafya. Hivyo huna ulazima wa kutafuta na kuhakikisha kwamba unavijumuisha vyakula hivyo katika lishe yako ya kila siku. Kwa sababu mwili wako una uwezo wa kutengeneza kwa kutumia vyanzo vingine vya viini lishe.

 

 

JINSI CHAKULA CHA MAFUTA KINAVYO MENG’ENYWA NA MPAKA KINAINGIA MWILINI

 

Umeng’enyaji wa vyakula vya mafuta huanzia kwenye sehemu ya mwanzo ya utumbo mwembamba iitwayo duodenum.

Na baada ya hapo rojorojo hutengenezwa ndani ya mfumo wa chakula yenye jina la kitalamu Micelles ndani yake kuna Mafuta (Fatty asidi na Gycerol), Lehemu,Vitamin Zinazo tembea na mafuta A,D,E na K huwa viko tayari kuingia ndani ya mwili wa binadamu.

Viini lishe hivyo huanza kufyonzwa na brashi za ukuta wa mfumo wa chakula na kuingia ndani ya seli za utumbo mwembamba (Enterocytes) na mara baada tu ya kupenyeza huungana tena kutoka kwenye ule mgawanyiko Fatty acid na Glycerol huungana tena kuwa Triacylglycerol (TAG). Hii ina maanisha kwamba Vyakula vya mafuta TAG vilimeng’enywa na kuwa Fatty acid na glycerol (Viini vidogovidogo) ili kuwezesha kupita kwenye kuta za mfumo wa chakula bila usumbufu. Lakini mara baada tu ya kupenyeza ukuta wa utumbo mwembamba huungana tena ili kuweza kusafirishwa kwenda sehemu mbalimbali za mwili.

Mfumo na njia za usafirishaji wa vyakula vya mafuta hutofautiana sana na vyakula vya wanga kwa sababu kiini lishe cha mwisho katika umeng’enyaji wa wanga ni glukosi (Sukari) ambayo ndio hupenyeza kuta za mfumo wa chakula hatimaye kuingia moja kwa moja kwenye mshipa wa damu uitwao hepatic portal vein ambao husafirisha chakula hicho kwenda moja kwa moja kwenye Ini kabla ya kupita sehemu nyingine yoyote ile.

Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba, sukari inapotoka kwenye utumbo mwembamba huenda moja kwa moja kwenye Ini la binadamu bila kupitia mzunguko mwingine wowote na husafirishwa na mfumo wa mzunguko wa damu. Ambapo vyakula vya mafuta huwa haviendi moja kwa moja kwenye Ini la binadamu isipokuwa baadhi tu kama Nazi (MCT) na mafuta husafirishwa na mfumo mwingine kabisa kutoka kwenye utumbo mwembamba huitwa lymphatic system.

Lakini vyakula vya mafuta huwa havipitii mlolongo wa kutoka kwenye utumbo mwembamba na kwenda moja kwa moja kwenye Ini isipokuwa baadhi tu ya vyakula vya mafuta ambavyo huwa vinafanyiwa kazi haraka sana na mwili kwa sababu maalumu ya muundo wake hurahisisha usafirishaji wake. Mfano Mafuta yote yenye muundo mdogo na wa kati huitwa Short Chain Fatty acid na Medium Chain Fatty acids. Mfano Nazi hupitia mlolongo ule wa kutoka kwenye kwenye utumbo mwembamba moja kwa moja hadi kwenye Ini. Hii ni kwa sababu ya umbo dogo kibaolojia vinaweza kubebwa kirahisi na mishipa midogomidogo inayopokea chakula Capillaries na kuupa mshipa mkubwa wa Hepatic portal vein. Lakini kuna aina nyingi ya mafuta hayawezi kupitia mlolongo huu kwa sababu hayawezi kubebwa ndani ya mishipa hio midogo lazima usafirishaji wake uwe kwa njia ya mirija inayo weza kusafirisha, Mfumo huo huitwa lymphatic system.

Hivyo basi mara baada tu ya Fatty acid na Glycerol, Lehemu pamoja na Vitamin A, D, E na K kupenyeza kutoka kwenye mfumo wa chakula na kuingia kwenye seli za utumbo mwembamba. Huungana na kutengeneza TAG ili iweze kusafirishwa vizuri ndani ya mirija ya mfumo wa Lymphatic ambao ni tofauti kabisa na mfumo wa mzunguko wa damu.

Kutoka hapo mafuta haya TAG hupokelewa na kibeba mafuta kiitwacho Chylomicrons ambacho huwa kimebeba shehena kubwa ya mafuta yote yaliyofyonzwa kutoka kwenye utumbo mwembamba. Kwa maana nyingine Chylomicrons ndio hubeba TAG na Lehemu kwenda sehemu mbalimbali za mwili pale ambapo kuna uhitaji wa nishati,cholesterol na kinachobaki huenda kutunzwa.

Hivyo basi Chylomicrons husafirishwa ndani ya mfumo tofauti na damu uitwao Lymphatic sytem, ambao nao una mirija yake maalumu iitwayo Lymph vessels (kama ilivyo mishipa ya damu). Chylomicrons inapokuwa imeanza safari yake kutoka kwenye mfumo wa chakula huwa imesheheni kiwango kingi sana (Tajiri) wa Mafuta TAG, vitamin A, D, E, K pamoja na Lehemu.

Kuhama kwa chylomiccron kutoka kwenye mfumo mmoja wa usafirishaji kwenda mwingine yaani kutoka mfumo wa lymphatic kwenda mfumo wa mzunguko wa damu hitimisho hilo hutokea kwenye mshipa wa damu mkubwa uitwao Subclavian vein na ndipo huanza kusafirishwa kwenda kwenye Ini la binadamu.

Baada ya kuingia kwenye mfumo wa damu na kabla ya kwenda kwenye Ini. Kadri chylomicron inavyosafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikifika kwenye tishu, Miili yetu imetengenezewa kimeng’enya kiitwacho Lipoprotein lipase ambacho huwa kinamegua mafuta TAG na kuyatumia pale yanapohitajika.

Kwa lugha nyingine pale mafuta yanapokuwa yamebebwa na Chylomicrons katika mfumo wa TAG huwa yanameguliwa na Kimeng’enya mafuta kiitwacho Lipoprotein lipase. Kadri mafuta yanavyozidi kumeguliwa kutoka kwenye kibebeo hicho ndivyo Chylomicrons inavyozidi kupungukiwa na TAG(Mafuta iliyobeba).

Je tishu za mwili wa binadamu hujipatia vipi mafuta kwa ajili wa nishati ya mwili?

Hujipatia kwa kutumia njia ya kumeng’enya au kumegua mafuta kutoka kwenye Chylomicrons ( kibeobeo kilicho na shehena na mafuta TAG) zoezi hizi huwezeshwa na kimeng’enya nilicho kitaja awali Lipoprotein lipase. Kwa hio kila kiungo chenye uhitaji wa TAG kitatumia njia ile ile kujipatia chanzo cha nishati wa mwili.

 

Baada ya mafuta kusafirishwa hadi kwenye Ini chylomicrons inafika kule ikiwa imebakiwa na kiwango kidogo sana cha mafuta TAG kwa sababu mafuta mengi imeyaacha njiani pale palipokuwa na uhitaji, ila pia itakuwa imebeba lehemu ndani yake kama nilivyo eleza mwanzo.

Baada ya mafuta kufikishwa kwenye Ini, Binadamu ametenegenezwa mfumo wa kusafirisha mafuta na lehemu kwenye damu. Hii ni kwa sababu asilimia kubwa ya damu ni maji ambapo huwezi kufanya zoezi la kuchanganya maji na lehemu/mafuta. Kwa lugha nyepesi ili kuwezesha mafuta kusafiri ndani ya mzunguko wa damu lazima yawezeshwe kuchangamana na damu ambayo asilimia kubwa ni maji.

Je Nini kinafanyika ili kuwezesha Lehemu/Mafuta yasafirishwe kwenye damu?

Ini la binadamu huwa linaanza kutengeneza visafirisha lehemu na mafuta viitwavyo Lipoprotein, Kama jina linavyosadifu, kwamba Lipoprotein ni muungano wa Mafuta (Lipid) na protini ndio maana jina la pamoja likawa Lipoprotein.

Kwa nini mafuta na lehemu hugubikwa (Coated) na protini ndipo yaweze kusafirishwa na damu?

Ili kuwezesha mafuta yaweze kuchangamana na damu lazima mafuta yafunikwe na protini na baada ya hapo damu itatumika kusafirisha lehemu au mafuta kwenda sehemu yenye uhitaji.

Jifunze kupitia mfano huu mzuri sana

Mtumbwi ukiwa umebeba abiria na unasafiri ndani ya mto mkubwa kama mto Nile. Ule mtumbwi ndio utakuwa Lipoprotein, abiria watakuwa ni lehemu na mafuta yaliyo bebwa ndani ya Lipoprotein na maji ya mto Nile ndio tunaweza kufananisha na damu.

Huu ni mfano tu ili upate picha ya kwamba Lehemu au mafuta huwa havisafirishwi kwenye damu moja kwa moja bali husafirishwa na vibabeo vya mafuta na lehemu viitwavyo Lipoprotein kwa lugha ya kingeleza chepesi unaweza kuita ni Cholesterol/Lipid containers (Kibebeo cha mafuta/lehemu).

 

 

 

 

AINA ZA VIBEBEO VYA LEHEMU NA MAFUTA MWILINI

Kuna aina kuu zifuatazo za visafirisha mafuta na lehemu vinavyotengenezwa na ini la binadamu ambavyo vinatengwa katika makundi mbalimbali kwa kutumia ukubwa wake unaopimwa katika kipimo cha density:

 1. Very Low Density Lipoprotein (VLDL)

Hiki ndicho hupokea mafuta na lehemu inayoletwa na Chylomicrons kutoka kwenye utumbo mwembamba mpaka kwenye Ini. Hivyo hupokea na kuanza kusambaza kule panapohitajika kwa matumizi mbalimbali.

 

 1. Intermediate Low Density Lipoprotein(IDL)

Hiki ni kibebeo cha lehemu na mafuta ambacho hupatikana pale Very Low density Lipoprotein (Kibebeo cha kwanza) kikaanza kupunguziwa mafuta pale yanapokuwa yanahitajika na kumeguliwa na kimeng’enya mafuta lipoprotein lipase.

Maana nyepesi hupatikana pale VLDL inapokuwa inashusha mzigo wa mafuta TAG kwenye tishu za mwili wa binadamu pale yanapokuwa yanahitajika kwa kazi mbalimbali za kiafya.

 

 1. Low Density Lipoprotein (LDL)

Hivyo hivyo kibebeo hiki kinapewa jina hili kadri Intermediate Low density Lipoprotein inavyozidi kushusha mzigo wa mafuta TAG na hatimaye kubakiwa na kiwango cha lehemu pekee.

Zingatia kwamba kadri vibebeo hivi vinavyoshusha mzigo wa mafuta TAG huwa vinapungukiwa mafuta na vinakuwa tajiri na lehemu.

Kumbuka kwamba LDL hufanya kazi sasa ya kusambaza lehemu (Cholestrol) popote pale katika mwili wa binadamu pale panapotokea na mapungufu na uhitaji mwilini ili kuendesha mwili wako.

 

Kwa sababu ya kupeleka lehemu kwenda sehemu inapo hitajika kutumika kimwili basi imepewa jina la “Lehemu mbaya” au Bad cholesterol ingawaje ubaya wake hadi sasa haujawahi kubainika kabisa kwa sababu kupeleka cholesterol penye uhitaji kisayansi sio kitendo kibaya kabisa ni kitendo salama kulingana na matakwa ya mwili kiafya.

 

Kwa maana hio kuita Low density Lipoprotein ni lehemu mbaya bado madaktari bingwa wa lehemu (Lipodologist) wanagoma. Ukisoma kitabu cha Prof Mary G Enig PHD, Ni Profesa wa Lehemu aliyepinga ugandamizwaji wa vyakula vya mafuta kwa sababu za kibiashara.Pia ameandika kitabu kiitwacho “Know Your Fats : The Complete Primer for Understanding the Nutrition of Fats, Oils” ameeleza kwa kina jinsi gani kiini lishe cha mafuta asilia kilivyorushiwa tuhuma ambazo hazina mashiko yoyote kisayansi.

 

Kitendo cha LDL kupeleka lehemu penye uhitaji sio kibaya kisayansi. Sababu ya LDL kuitwa ni lehemu mbaya nadhani ni kwa sababu ya tafiti mbalimbali zilizolenga kugandamiza vyakula vya mafuta na kuongeza nguvu soko la sukari na wanga

 

 1. High Density Lipoprotein (HDL)

Hiki pia ni kisafirisha lehemu ambacho huwa kina uhaba wa lehemu ndani yake sio kama visafirisha lehemu vingine ambavyo vina utajiri (Vimesheheni mafuta na lehemu).

 

Kwa sababu ya uhaba huo hutumika kubeba lehemu kutoka sehemu mbalimbali na kurudisha kwenye Ini lako kwa matumizi mengine au kutolewa nje kwa njia ya nyongo.

Kutokana na masomo yetu ya kila siku tunafundishwa kwamba HDL ni lehemu nzuri “Good Cholesterol” uzuri wake ni kwa sababu ya upungufu wa lehemu na kwa maana hio ina nafasi kubwa hukusanya lehemu kutoka kwenye mishipa ya damu na kurudisha kwenye Ini lako.

 

Kisayansi hakuna cholesterol mbaya wala nzuri. Na hata vibebeo vya cholesterol iwe LDL au HDL hakuna kizuri wala kibaya. Vyote vinafanya kazi kutimiza matakwa ya mwili kibaolojia. Bila hivyo kutenda kazi hizo hauwezi kuwa na uhai.

 

Kufupisha maelezo jinsi mafuta na lehemu inavyosafirishwa:

 

TAG na Lehemu kutoka kwenye Utumbo mwembamba, Hubebwa na Chylomicrons,Kisha hupokelewa na VLDL kwenye Ini lako, Baada ya hapo VLDL inaanza kupeleka kule Mafuta yanapohitajika na kule lehemu inapo hitajika, Inapokuwa inapeleka inakuwa inatua mzigo wa mafuta na lehemu. Hivyo VLDL inaanza kubadilisha majina kutokana na kiwango cha mafuta na lehemu inavyotua. Itatoka kuwa VLDL ,Kisha LDL na Mwisho Kabisa HDL.

 

Ndivyo mafuta yanavyo safirishwa katika mwili wa binadamu kuanzia unavyokula hadi kuingia ndani ya mwili wako.

 

FIKRA POTOFU AMBAZO ZIMEJENGEKA

 

 1. Vyakula vya mafuta hurundikana mwilini kama mafuta. Ni uongo mkubwa sana kuna nyakati chache sana kibaolojia ambazo hutokea mafuta yakarundikwa kama mafuta. Asilimia kubwa hapana. Na kumbuka kwamba kitendo cha uhifadhi wa mafuta mwilini husanifiwa na vichocheo vya mwili, ambapo hapa insulin ndio huhamasisha mafuta kuhifadhiwa na inapopungua huruhusu mafuta kuunguzwa.

Vyakula vya mafuta havina uwezo mkubwa wa kuchokoza kongosho kumwaga homon hii inayonenepesha na kutuzuia kupungua kama ilivyo vyakula vya wanga na sukari.

 

 1. Vyakula vya mafuta vinaongeza Lehemu mbaya mwilini mwako. Hapana hakuna ukweli katika hili kisayansi. Kwanza misingi ya sayansi hakuna sehemu yoyote inapo onesha muundo wa mafuta yanayo ganda yanaweza kubalika na kuwa cholesterol. Aliyetuambia hilo alihusianisha tu kitafiti na hakuna ushahidi wowote wa misingi ya sayansi. Vitabu vyote vya lishe na muundo wa viini lishe (Biochemistry) vinakanusha hilo.

Pili kitabu cha Guyton Medical physiology Eleventh edition kinakanusha ya kwamba cholesterol unayokula ni sawa na cholesterol itakayo ingia kwenye damu. Kadri unavyokula cholesterol mwili huwa una namna ya kuzuia ongezeko hilo kwa kuzuia utengenezaji wa cholesterol kwenye Ini kusitishwa. Kitendo hiki hufanyika kwa ongezeko la lehemu kwenye damu huenda kuzuia 3 hydroxy 3 methylglutaryl CoA Reductase ambayo huhusika na kuratibu utengenezaji wa cholesterol mwilini.

 

Kwa lugha nyepesi “Ukila cholesterol nyingi mwili utatengeneza kidogo, na ukila kidogo mwili utatengeneza kuziba pengo hilo, kutokula vyakula vya cholesterol kwa lengo la kupunguza cholesterol ni kazi bure kwa sababu mwili huwa una uwezo wa Zaidi ya asilimia 80 kutengeneza cholesterol

 

 1. Jamii inashindwa kutofautisha kati ya mafuta mabaya na mazuri. Hakuna ubaya wa mafuta asilia kama nyama, mayai, siagi, nazi, parachichi lakini kuna ubaya pale unapoingia mkono wa binadamu kututengenezea mafuta na kuyaita mazuri. Mafuta kama Margarine, ambayo tunatumia katika vyakula vyetu kila siku kupaka kwenye mikate, kupikia keki, mikate, mandazi.

 

Epuka mafuta ya mkono wa binadamu. Ila kwa sababu jamii imeanza kutambua ubaya wa margarine, siku hizi margarine jina limepitwa wakati wanaita, Transfats, wengine wanakuficha zaidi Partially hydrogenated oils kumaanisha kitu kilekile. Viwanda vinajua ubora wa margarine inapowekwa kwenye bidhaa haziharibiki mapema ndio maana majina yanabadilishwa kwa sababu kwao inawanufaisha ila mlaji anaumia.

Ili uwe mzima wa afya njema kuwa makini na chakula unachokula popote soma kwa makini au ulizia jinsi kilivyo pikwa. Vyakula kama keki, mandazi, vitafunwa vya aina yoyote ile, mikate jitahidi sana kuepuka vyakula hivyo pale unapokuta vimepikiwa mafuta hayo.

 

 

 

USAFIRISHAJI WA LEHEMU (CHOLESTROL) MWILINI

 1. Kipimo cha Lehemu ambacho unaweza kukiita ni kipimo kilicho boreshwa zaidi ya kile cha awali chenye kuonesha jumla ya lehemu pekee. Kipimo hiki kitalamu huitwa “Ordinary Lipid Profile test” kinatupa picha kiundani ya viashiria vyote vinavyohusika na kutoa maelezo kuhusu afya yako ukizingatia mafuta ndani ya mwili wako.

 

Lehemu katika mwili wa binadamu huwa haisafiri yenyewe kama ilivyo bali huwa inabebwa na kitu kitwaacho “Lipoprotein” kutoka sehemu moja kwenda panapotakiwa ifike.

 

Kumbe ina maana kwamba nikitafuta lehemu kwenye damu sitaikuta ila nitaikuta ndani ya vibebeo vya lehemu “Cholesterol Containers” kwa jina la kisayansi Lipoprotein!

 

Lehemu hubebwa na lipoprotein kwa sababu lehemu huwa ina sifa kama ya mafuta  ya kutochangamana na damu kwa sababu asilimia kubwa ya damu ni maji,hio ndio sababu kwamba lehemu haisafirishwi kwenye damu jinsi ilivyo lazima igubikwe (Ifunikwe) na protini ambazo ndizo zinawezesha lehemu kusafiri kwenye damu.

 

Hivyo basi ili lehemu isafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine husafiri katika mfano wa unavyosafirisha mzigo wako kuvuka mto kwa kutumia mtumbwi. Ule mtumbwi ndio kisafirisha lehemu na mzigo ndio lehemu hebu weka mtizamo huo kichwani mwako halafu utanielewa ninaposema lehemu husafirishwa kwenye damu katika mfumo wa vibebeo na sio kama ilivyo yenyewe.

 

Hivyo basi lehemu hupewa jina la “Lipid” yaani “Mafuta” kama tulivyojifunza hapo awali. Hivyo ili lehemu isafirishwe huwa inafunikwa kwanza na protini ndio maana muungano kati ya lehemu na protini tunapata “Lipoprotein” ambayo imepatikana kwa “lipid +protein=Lipoprotein”.

 

Umeona sasa jina hili linapotokana? Na ukisikia lehemu katika mwili wa binadamu kinachotakiwa kugonga kwenye kichwa chako huwa inasafirishwa na kitu ambacho jina lake ni “Lipoprotein”.

 

 

 

 

Kumbuka sasa Lipoprotein huwa zinachanganuliwa kutokana na ukubwa wake katika kipimo cha “Density” na kiwango cha mafuta na lehemu kilivyobeba. Rejea somo letu la awali kama umesahau jinsi mafuta na lehemu inavyo safirishwa katika mwili wa binadamu.

 

Haya funga mkanda tena tunaingia kwenye misingi ya sayansi ambayo huwa haisemi uongo kabisa ukinielewa hapa basi hautakuwa na woga katika utekelezaji wa masomo haya:

 

Lehemu huwa inasafirishwa na visafirisha mafuta na lehemu vyenye majina yafuatayo:

 

 • Chylomicrons

 

Hivi ni visafirisha lehemu na mafuta ambavyo hutengenezwa na utumbo mwembamba na ndivyo mara baada tu ya mafuta na lehemu kupenyeza utumbo mwembamba ili kusafirishwa hubebwa na chylomicrons.

 

Ndio maana mara baada tu ya kula kiwango cha Chylomicrons huwa ni kikubwa sana endapo ukipima kwa kutumia sampuli ya damu, maana huashiria kwamba kinafanya kazi yake ya kusafirisha mafuta kutoka kwenye utumbo mwembamba na kuingiza kwenye mfumo uitwao “Lymphatic system”.

 

Nilifundisha mwanzo kwamba vyakula vya wanga na sukari hufyonzwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye Ini la binadamu kwanza kupitia mshipa mkubwa wa damu uitwayo Hepatic portal vein lakini vyakula vya mafuta na lehemu isipokuwa yenye aina flani ya mafuta kama nazi ambayo hujulikana kama Medium chain Fats hupenya moja kwa moja na ndio maana hutumika sana kubusti shughuli za mwili kwani mwili unavuna mapema sana nishati inayotokana na mafuta ya nazi (MCT) ukilinganisha na mafuta mengine. Lakini mafuta mengine yote huwa yanapitia mlolongo mlefu kwanza kabla ya kuingia kwenye damu.

 

Kwa hio chylomicrons huwa ni tajiri wa mafuta na lehemu ambapo kadri inavyotoka kwenye utumbo mwembamba huwa inaenda inatua mafuta kwa kitendo cha mafuta kumeguliwa na kimeng’enya kiitwacho Lipoprotein lipase ambacho huwa kipo kwenye tishu za mwili.

Sababu ya tishu za mwili kuwa na lipoprotein lipase ni kuwezesha kumegua mafuta kwa matumizi maalumu penye mahitaji.

 

Chylomicrons huendelea kusafiri mpaka inapoingia kwenye mfumo wa mzunguko wa damu kutoka mfumo mwingine lymphatic system huingilia kwenye mshipa mkubwa wa damu uitwayo Subclavian vein kwa kutumia mrija uitwao Thoracic duct. Hatimaye huenda mpaka hitimisho la safari yake kwenye Ini.

 

Kwa hio chylomicrons husafirisha mafuta na lehemu kutoka kwenye utumbo mwembamba mpaka kwenye Ini la binadamu. Baada ya hapo huhifadhiwa na vibebeo vingine viitwavyo “Very Low density Lipoprotein”

 

 • Very Low density Lipoprotein (VLDL)

 

Hivi ni vibebeo vya lehemu na mafuta katika mfumo wa TAG (Triacylglycerol) ambavyo hutengenezwa na ini la binadamu. Kazi yake ni kusafirisha lehemu na mafuta pale yanapohitajika.

 

Kumbuka Miili yetu imetengenezwa ya kwamba zaidi ya asilimia 80 ya lehemu katika mwili wa binadamu hutengenezwa ndani ya mwili wako. Kwa hio chanzo kikuu cha lehemu katika mwili wako ni mwili wako na sio chakula. Mwili unategemea kiwango kidogo sana cha lehemu kutoka kwenye vyakula. Hivyo chakula sio chanzo kikuu cha lehemu katika mwili wa binadamu.

 

Ndio maana katika tendo la kuhakikisha lehemu haizidi mwili huwa unasanifu ufyonzaji wa lehemu kwa umakini mkubwa sana “Lehemu nyingi ikiingia kupitia chakula mwili utaitikia kwa kutengeneza kidogo”

 

Sivyo kama tunavyodanganywa kwamba “Kwa sababu mwili unatengeneza lehemu wenyewe huna haja ya kuupa lehemu unaufanya mwili wako kulemewa lehemu” Sio ukweli kwani “Mwili ukiunyima utatengeneza kufidishia kiwango kilichopungua na mwili ukiupatia utatengeneza kile kidogo kilichopungua” kwa hio kutokula au kula hakuwezi kubadilisha lolote kwenye damu kama tunavyojidanganya n ahata kama mabadiliko yakitokea huwa ni madogo sana kisayansi!

 

Baolojia haijawahi kubadirika ila binadamu huibadilisha kwa maslahi binafsi.

 

Hivyo basi VLDL inapotoka kwenye ini na kupeleka lehemu na mafuta kwenda kule kunapohitajika kadri inavyosafiri inakuwa inatua mzigo iliyobeba ambao ni lehemu na mafuta. Na kadri inavyopunguza mzigo inakuwa inabadilisha majina yake kwa sababu ukubwa wake unapungua. Ndio maana tunapata kibebeo kingine kinaitwa Intermediate density Lipoprotein (IDL) hiki kinapatikana kutoka kwenye VLDL. Zoezi hili linaendelea mpaka tunapata kisafirisha lehemu kiitwacho Low density Lipoprotein (LDL) hiki huwa kinakiwango kingi cha lehemu ambacho kimebeba kupeleka sehemu inapo hitajika.

 

 • Low Density Lipoprotein (LDL)

Kibebeo hiki huwa ni “tajiri wa lehemu” ambayo imebebwa kwenda sehemu husika. Kinajulikana sana katika ulimwengu wa tafiti za kisayansi kwa jina maarufu “Lehemu mbaya” au “Bad cholesterol”. Kumbe sasa unatakiwa utambue kwamba jina la Lehemu mbaya kutumika mbadala wa jina halali LDL linaifanya jamii ione kwamba LDL ndio adui anaye tuuguza.

 

Swali la kujiuliza kwa nini kibebeo hiki kilipewa jina la lehemu mbaya?

 

Jibu ni kwa sababu husafirisha lehemu kwenda sehemu inapohitajika! Yaani kutoka kwenye Ini lako kwenda kwenye tishu za mwili wako kule inapohitajika kupitia mishipa ya damu. Huo ndio ubaya wake! Yaani imepewa jina baya kwa sababu ya kutekeleza majukumu yake.

 

Kwamba, Unapokula vyakula vya mafuta kama nyama, siagi, parachichi, nazi mayai unaongeza lehemu mbaya (LDL) unapunguza lehemu nzuri (HDL) na matokeo yake unakuwa hatarini kupata magonjwa ya moyo. Usistuke ndivyo tunavyodanganyika!

 

Ukweli ni kwamba unapokula vyakula vya mafuta asilia kama nyama mayai,parachichi,nazi unaongeza kiwango cha lehemu nzuri ijulikanayo kama HDL na kama ikienenda na kupunguza sukari pamoja na wanga mbaya kama mikate,mandazi,keki,soda,juisi,wali nk utakuwa umepunguza uwezekano wa wewe kuugua magonjwa ya moyo.

 

Kwani hata kama kiwango cha Lehemu mbaya LDL inayosakika kuongezeka kinacho ongezeka ni LDL ambazo ni chembe kubwa ambazo hazina madhara na wala sio zile ndogo ambazo zina madhara makubwa na huongezeka kwa kasi sana pale unapokula wanga na sukari kupindukia. Ndio maana tafiti nyingi zinaonesha kwamba hakuna faida yoyote ya kuacha vyakula vya mafuta na kuanza kula wanga na sukari kupindukia utakuwa unaweka mwili wako hatarini sana kupata magonjwa ya moyo. Jamii yetu ipo katika hali hii lakini bado inashangaa adui yupi! Ni sukari na wanga mtambue kuanzia leo.

 

Nitajadili kipimo kingine kizuri zaidi ya Ordinary Lipid Profile test kinaitwa “Advanced Lipid Profile test” ambacho kwa Tanzania hospitali chache sana wanakitumia hicho ndicho kinakupa picha kamili kuhusu ukweli wa hali yako kiafya na sio hivi.Hospitali nyingi zinatumia kipimo cha kuonesha lehemu iko juu au hapana hata kwenye kiwango cha kutumia “Ordinary Lipid profile test” hazijafikia. Kuwa makini unapochagua kipimo kinachokuweka kwenye dawa, Chaguo la kipimo sahihi ni muhimu sana ili kuepusha kuhatarisha mwili wako na dawa za kushusha lehemu pasipokuwa na sababu nzito au ya msingi.

 

 • High Density Lipoprotein

 

Hii hujulikana kwa herufi tatu kama HDL, jina la kisayansi katika tafiti mbalimbali utasikia inatamka “Lehemu nzuri” yaani “Good Cholesterol”.

 

Kupewa jina hili kwamba ni lehemu nzuri ni kwa sababu kazi yake katika mwili wa binadamu “Huwa ni kuchukua lehemu ambayo haitumiki kutoka sehemu mbalimbali za mwili wako ikiwemo mishipa ya damu na kupeleka kwenye Ini la binadamu kwa lengo la kuhifadhi au kutoa nje ya mwili wako kupitia nyongo ndani ya haja kubwa.

Ndio maana ikapewa jina la lehemu nzuri.Lakini ukija kibaolojia zote HDL na LDL zipo katika mwili wa binadamu kutimiza malengo yake kama kawaida lakini sasa sisi tumechukulia ya kwamba lehemu mbaya (LDL) haitakiwi hata kuwepo mwilini ambayo sio kweli kabisa.

 

MAPUNGUFU YA KIPIMO NA ELIMU YA LEHEMU

 

 1. Jumla ya lehemu huwa inachukuliwa kigezo toshelevu cha mtu kuanza dawa pale inapoonekana ipo kiwango cha juu kulingana na kiwango kinachotakiwa kuwa.

Lakini ukweli ni kwamba tafiti zinakataa kutumia kigezo hicho kimoja pekee kumwanzishia dawa mtu za kushusha lehemu kutokana na athari zake na gharama zake ni bora apate ushauri jinsi ya kutunza mwili wake kiafya kwa lishe na mitindo mingine ya maisha.

 

 1. Kiwango cha mafuta (TGA) kikiwa kingi kwenye damu wakati kipimo kinafanyika hutumika pia kumwambia mgonjwa kwamba ana mafuta mabaya mengi anatakiwa apunguze kwa dawa.

Lakini ukweli ni kwamba ili upate kiwango sahihi cha mafuta haya (TGA) yanayotoka kwenye Ini hakikisha kwamba unapoenda kupima kipimo hiki uwe hujala chochote kuanzia masaa 12 na kuendelea. La sivyo utapata jibu la uongo kwa sababu mara tu tunapomaliza kula ukipima kiwango cha TGA lazima utakikuta kipo juu. Lakini haimaanishi natakiwa dawa.

 

Ni sawa na mtu ameenda kupima ugonjwa wa UTI bila kupewa masharti aina gani ya mkojo anakalete basi yeye anaenda kukusanya mkojo wowote ndipo akileta mkojo wa kwanza kutoka lazima kipimo kitatoa majibu ya uongo. Ila ungempatia maelekezo mazuri achukue mkojo wa katikati basi ungemwepusha na dawa zisizo na msingi na ungebaini kisababishi kingine cha homa.

 

Kumbuka pia, endapo ukikaa masaa 12 ndio ukapata kipimo hiki kitakuonesha kiwango cha mafuta haya ambayo haimaanishi kwamba yamehifadhiwa kwa kula vyakula vya mafuta hapana! Vyakula vya wanga na sukari ndivyo huhifadhi mafuta kwenye Ini kwa kiwango kikubwa. Lakini utashangaa ushauri hutapewa kuacha vyakula vya sukari, chapati ,keki,soda ila utaambiwa acha nyama,mayai,nazi,parachichi vyakula ambavyo havina hatia ya moja kwa moja.

 

 

Profesa Stephen phinney alishawahi kufanya tafiti kwa kumpatia mtu aliyejitolea kwa utafiti. Chakula cha wanga na chakula cha mafuta katika kiwango sawa. Halafu akapima POA (Palmitic Oleic Acid) ambacho ni kiashiria cha mrundikano wa mafuta mwilini. (10)

 

Alichokibaini ni kwamba yule aliyekula wanga alionesha kiwango kikubwa cha POA kuliko aliyekula chakula cha mafuta. Hii ina maana vyakula vya wanga na sukari unatakiwa uvitizame kwa jicho pevu na woga mkubwa sana vina uwezo sio tu kukunenepesha ila kukuweka hatarini na magonjwa ya kisukari na moyo.(11) (12) (13)

 

 

 

 

 

 • Kiwango cha LDL (Lehemu mbaya) na HDL (lehemu nzuri)

Hiki pia kimekuwa kikitumika kama kigezo cha watu wengi kuwa katika mzigo wa dawa za kushusha lehemu.

Kiwango kingi cha LDL na kiwango kidogo cha HDL hali hio inakufanya kuwa hatarini kupata magonjwa ya moyo. Hivi ndivyo tunavyo ambiwa.

Ukweli ni huu, Kiwango kingi cha LDL huongezwa kwa kasi na uhujumu wa sukari na wanga, na katika kipimo ambacho ni kikubwa zaidi nitakachokufundisha ni kwamba wanga na sukari huongeza LDL ambazo ni chembe ndogo sana katika ukubwa na kukufanya kuwa hatarini sana kupata magonjwa ya moyo.

Wakati vyakula vya mafuta kama nyama, mayai, nazi siagi huongeza LDL lakini ni Chembe Kubwa ambazo huwa hazisababishi magonjwa ya moyo. Katika kipimo hiki huwezi kupata ufafanuzi huo.

Kumbuka hakuna dawa duniani ya kuongeza LDL ila dawa nzuri kabisa ya kuongeza lehemu nzuri ni kuacha kuhujumu vyakula vya wanga na sukari,tumia mafuta ya,Olive oil,Nazi,samaki,nyama ya ng’ombe wakufuga,mafuta ya karanga mbalimbali kama Flaxseed,almonds,korosho nk.

LDL lazima ipate udhuru ndani ya mishipa ya damu ndipo inaweza kusababisha magonjwa ya moyo. Bila hivyo haiwezi kuleta madhara yoyote katika mwili wa binadamu. Na moja ya sababu kubwa inayoleta udhuru katika LDL na kisha kusemekana ni cholesterol mbaya ni vyakula vya sukari na wanga, mafuta mabaya yaani margarine, nk (14)

 

 1. Kipimo hiki sio toshelevu kwa sababu

Tunaposema HDL maana yake ni kiwango cha lehemu kilichobebwa ndani ya kibebeo hiki HDL na sio idadi ya HDL. Hivyo hivyo tunaposema kwamba LDL ni nyingi tunaamanisha kwamba, Kiwango cha lehemu kilichobebwa ndani ya LDL ni nyingi ila sio “Idadi ya LDL”.

Chukua mfano, LDL si ndio tunasema ni lehemu mbaya. Sasa chukulia mfano kuna gari Landcruzer moja, ila imebeba watu 10 ndani yake. Hao watu wanakuja wote kukushambulia na wamebeba silaha. Kwa maana hio Gari moja itakuwa na maadui 10 ndani yake. Halafu tena chukua mfano kuna Landcruzer 20 kila gari imebeba maadui 10 ina maana kwamba kutakuwa na maadui 200 katika gari 20. Je wewe kama unataka kupima uzito wa maadui wanaokuja kukuangamiza msafara upi utauogopa? Jibu lazima uwe ni msafara wa magari 20 wenye maadui 10 ndani yake. Kwa maana yake tunachotakiwa kingine kuangalia ni “IDADI YA WABEBA MAADUI NA SIO WAMEBEBA MAADUI WANGAPI” .

Kwani nitakushangaa unaogopa msafara wa gali moja lenye watu 200 kuliko msafara mmoja wenye magari 20 na umebeba maadui 10.

Namaanisha nini? Kwamba, Tunatakiwa tuwajue maadui wetu wapo wangapi kiujumla kitalamu tunaita “Lipoprotein Particles” na sio kiwango cha lehemu pekee. Kwa maana hio itatakiwa tuhame kutoka kwenye kuangalia kiwango cha lehemu kilichobebwa na LDL au HDL na tuangalie idadi ya LDL na HDL.

Kipimo chetu cha kawaida ordinary Lipid Profile Test hakiwezi kutupa majibu hayo ndio maana sasa hospitali nyingi zinatumia kipimo sahihi zaidi kiitwacho “Advanced Lipid profile test” kinakupa ukweli zaidi na kiko kisasa zaidi.

Katika kipimo hicho utakutana na maneno haya:

LDL-Particles, HDL-Particles, Small LDL Particles,Large LDL particles kumaanisha kwamba huu ndio ufafanuzi wa kisasa. Ukiambiwa kiwango cha lehemu yako mbaya LDL-C kiko juu, Hakikisha unafanya kipimo hiki “Kikubwa zaidi” tafuta sehemu yoyote kwenye hospitali kubwa upime. Itakupa idadi ya LDL na sio kiwango cha lehemu ndani yake.

Sio hivyo tu itakwambia ni LDL particle zipo ngapi,na je Kubwa au ndogo ndizo ziko juu? Yaani (small LDL au Large LDL)?

Kumbuka kwamba unaweza kukuta kwamba una kiwango kingi cha LDL lakini kumbe ni Large LDL na hauko hatarini katika kupata magonjwa ya moyo. Tafiti zinaonesha kwamba mtu ambaye anachukia wanga na sukari na anakula vyakula kama samaki,Nazi,mayai,mboga za majani matunda atajikuta kwamba akipima kipimo hiki atakuta kiwango cha LDL kipo juu,lakini akiendelea kupima atakuta Large LDL ndio iko juu na sio Small LDL.(15) (16)

Note: Pia Small LDL huwa inatumiwa kwa jina jingine kumaanisha ni sawa na Apo B. hivyo ukikuta kwenye kipimo usishangae.

Hivyo basi kumbuka vyakula vya wanga na sukari kwa anaye hujumu vinavyongezea kiwango cha LDL hasa vile vihatarishi vikubwa kabisa viitwavyo Small LDL ambavyo ndio ni virahisi sana kupenyeza na kwenda kurundikana kwa kutengeneza donge na lehemu ndani ya kuta za mshipa wa damu pale penye jeraha.

 

REJEA ZA MAKALA HII

 1. Lipid peroxidation in culinary oils subjected to thermal stress.
 2. Dhalla NS, Temsah RM, Netticadan T. Role of oxidative stress in cardiovascular diseases. J Hypertens. 2000 Jun;18(6):655–73.
 3. Cervantes Gracia K, Llanas-Cornejo D, Husi H. CVD and Oxidative Stress. Journal of Clinical Medicine. 2017 Feb 20;6(2):22.
 4. Csányi G, Miller FJ. Oxidative Stress in Cardiovascular Disease. Int J Mol Sci. 2014 Apr 9;15(4):6002–8.
 5. Fearon IM, Faux SP. Oxidative stress and cardiovascular disease: Novel tools give (free) radical insight. Journal of Molecular and Cellular Cardiology. 2009 Sep 1;47(3):372–81.
 6. Chowdhury R, Warnakula S, Kunutsor S, Crowe F, Ward HA, Johnson L, et al. Association of dietary, circulating, and supplement fatty acids with coronary risk: a systematic review and meta-analysis. Ann Intern Med. 2014 Mar 18;160(6):398–406.
 7. Schwingshackl L, Hoffmann G. Dietary fatty acids in the secondary prevention of coronary heart disease: a systematic review, meta-analysis and meta-regression. BMJ Open. 2014 Apr 1;4(4):e004487.
 8. Siri-Tarino PW, Sun Q, Hu FB, Krauss RM. Meta-analysis of prospective cohort studies evaluating the association of saturated fat with cardiovascular disease. Am J Clin Nutr. 2010 Mar 1;91(3):535–46.
 9. Souza RJ de, Mente A, Maroleanu A, Cozma AI, Ha V, Kishibe T, et al. Intake of saturated and trans unsaturated fatty acids and risk of all cause mortality, cardiovascular disease, and type 2 diabetes: systematic review and meta-analysis of observational studies. BMJ. 2015 Aug 12;351:h3978.
 10. The Art and Science of Low Carbohydrate Living An.
 11. Associations of fats and carbohydrate intake with cardiovascular disease and mortality in 18 countries from five continents (PURE): a prospective cohort study – The Lancet [Internet]. [cited 2018 Jul 21]. Available from: https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(17)32252-3/abstract
 12. Sugar consumption plays greater role in heart disease than saturated fat [Internet]. ScienceDaily. [cited 2018 Jul 21]. Available from: https://www.sciencedaily.com/releases/2016/01/160113103318.htm
 13. Mozaffarian D, Rimm EB, Herrington DM. Dietary fats, carbohydrate, and progression of coronary atherosclerosis in postmenopausal women. Am J Clin Nutr. 2004 Nov;80(5):1175–84.
 14. Parthasarathy S, Raghavamenon A, Garelnabi MO, Santanam N. Oxidized Low-Density Lipoprotein. Methods Mol Biol. 2010;610:403–17.
 15. Arsenault BJ, Lemieux I, Després J-P, Wareham NJ, Luben R, Kastelein JJP, et al. Cholesterol levels in small LDL particles predict the risk of coronary heart disease in the EPIC-Norfolk prospective population study. Eur Heart J. 2007 Nov 1;28(22):2770–7.
 16. Cromwell WC, Otvos JD, Keyes MJ, Pencina MJ, Sullivan L, Vasan RS, et al. LDL Particle Number and Risk of Future Cardiovascular Disease in the Framingham Offspring Study – Implications for LDL Management. J Clin Lipidol. 2007 Dec 1;1(6):583–92.

—————————————————————————————————————————————–

 

NB: Pata Nakala ya Sayansi ya Mapishi kitabu ambacho kimewasaidia maelfu na maelfu ya Watanzania Kutimiza malengo kiafya. Hutajutia kusoma na Kuyaamini niliyo andika kwa kutumia tafiti mbalimbali.

No automatic alt text available.

Pia Kitabu cha wagonjwa wa kisukari na mtu yeyote anayetaka kujikinga na ugonjwa wa kisukari Kipo sokoni unaweza kuwasiliana nasi ukapata nakala yako ukasoma kwa kina kabla hujaugua ugonjwa wa kisukari na kama tayari umesha ugua inaweza kuwa ni msaada kwako.

Image may contain: text

 

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*